Aidan Mtakatifu
From Wikipedia
Aidan Mtakatifu wa Lindisfarne (pia huitwa Mtume wa Northumbria) alianzisha kituo cha utawa na kuwa askofu wake wa kwanza kwenye kisiwa cha Lindisfarne kule Uingereza. Alifariki kule Northumbria 31 Agosti, 651. Anaheshimiwa kufufua Ukristo katika eneo la Northumbria. Alikuwa ametoka Ireland, na kabla hajaja Northumbria alikuwa mtawa katika kituo cha utawa kwenye kisiwa cha Iona kule nchi ya Scotland.
Wakati wa enzi ya Warumi, Ukristo ulikuwa umeenea mpaka Uingereza, lakini kwa sababu ya kushindwa kwao Warumi, upagani ukaanza kurudi upande wa kaskazini wa Uingereza. Oswald, mfalme wa Northumbria, mwaka wa 616 BK alilazimishwa kwenda uhamishoni kule kisiwa cha Iona ambako akabadili kuwa Mkristo na kubatizwa. Mwaka wa 634 Oswald alirudishiwa ufalme wa Northumbria na akaamua kuwaingiza katika Ukristo wananchi wake ambao wengi wao walikuwa wapagani. Ili kutekeleza lengo hilo aliwaomba watawa wa Iona wamtumie wamisionari. Naye Aidan akafika mwaka wa 635.
Aidan alichagua kisiwa cha Lindisfarne kiwe makao makuu ya dayosisi yake kwa vile kilikuwa karibu na ngome ya kifalme kule Bamburgh. Mwanzoni ilikuwa mfalme Oswald mwenyewe aliyewatafsiria Aidan na watawa wake kwa vile walikuwa hawajajifunza Kiingereza. Baada ya kifo chake Oswald mwaka wa 642, Aidan alisaidiwa na mfalme Oswine wa Deira, nao wakawa marafiki wa karibu sana.
Aidan alikuwa huwatembelea watu kijiji hadi kijiji, kuongea nao kiadabu na kujaribu katika maongezi hayo wavutwe na Ukristo. Kufuatana na hadithi moja, mfalme alimpa Aidan farasi ili asihitaji kutembea kwa miguu lakini Aidan akatoa farasi tena kama zawadi kwa mtu maskini.
Aidan aliweza kuongea na watu walioko na hivyo alifaulu kuwasaidia wananchi wengi wa Northumbria wawe Wakristo. Pia katika kituo chake cha utawa aliwafundisha wavulana kuminawawili, wenyeji wa Northumbria, ili kuhakikisha kwamba kanisa la Uingereza liongozwe na Waingereza wenyewe.
Aidan alifuata tawi la Ireland la Ukristo siyo tawi la Roma. Hata hivyo tabia yake na bidii ya katika umisionari zilisababisha na Papa Honorius I alimheshimu. Kituo cha utawa cha Lindisfarne kiliendelea kukua na kuanzisha makanisa na vituo vingine. Pia kilikuwa kama hazina ya ujuzi wa kitaalamu. Baadaye, Bede Mtakatifu aliandika wasifu ya maisha yake Aidan pamoja na miujiza yake yote. Sikukuu yake Aidan Mtakatifu ni tarehe 31 Agosti.
[edit] Marejeo ya nje
- Irelandseye.com wasifu ya maisha yake Aidan Mtakatifu
- Saint Aidan of Lindisfarne ilivyoandikwa na Mch. Kate Tristram
- Britannia wasifu ya maisha yake Aidan Mtakatifu
- Historia ya Kanisa (katika nyakati za Aidan) ilivyoandikwa na Philip Hughes