Dar es Salaam
From Wikipedia
Dar es Salaam ni jiji kubwa kuliko yote nchini Tanzania. Ni pia jina la Mkoa wa Dar es Salaam. Hali halisi ni pia mji mkuu wa Tanzania hata kama Dodoma imetangazwa kuwa mji mkuu tangu mwaka 1973. Lakini ofisi za rais na wizara nyingi bado zinafanya kazi Dar es Salaam ambayo hali halisi ni makao makuu ya serikali.
Jiji hili zamani liliitwa Mzizima. Sultani Seyyid Majid wa Zanzibar ndiye aliyelipa jiji hili jina linalotoka kwenye Kiarabu (دار السلام Dār as-Salām)lenye kumaanisha "Nyumba ya Amani." Maelezo yanayopatikana mara nyingi kuwa maana ni "Bandari ya Salaam" inachanganya maneno mawili yanayofanana ya "dar" (=nyumba) na "bandar" (=bandari).
Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni tatu. Ingawa Dodoma inafahamika kama ndio mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam ndiko ziliko ofisi kuu za viongozi wa serikali, mabalozi, mashirika ya kimataifa, n.k. Bandari ya Dar es Salaam katika bahari ya Hindi, ndio bandari kubwa nchini Tanzania inayojihusisha na usafirishaji na uingizaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji, ujenzi, magari, madawa, n.k.
Kiutawala, Dar es Salaam imegawanywa katika wilaya za Temeke, Ilala, na Kinondoni.