Boksiti
From Wikipedia
Bauxiti au Boksiti ni mtapo unaotumiwa kutengeneza alumini. Ni hasa hidroksidi ya alumini (Al2O3.3H2O) ikichanganywa na titani, chuma au silikoni.
Jina la Bauxiti limetokana na kijiji cha "Les Baux de Provence" katika Ufaransa ambako mtapo umegunduliwa mara ya kwanza. Leo hii huchimbwa hasa katika Australia, Brazil, Guinea, Jamaika na India.
Bauxiti ni msingi wa alumini na mambo yote yanayotengenezwa nayo. Kama metali imara na nyepesi alumini hutumiwa hasa kwa ndege na vyombo vingine vya usafiri lakini pia kwa ajili ya makopo, masanduku n.k. Matengenezo ya alumini kutokana na bauxiti huhitaji nishati nyingi hasa ya umeme. Kwa sababu hiyo viwanda vya alumini hujengwa karibu na vituo vya umeme na hii ni sababu ya kwamba nchi penye bauxiti haziwezi kufaidika na viwanda vyenyewe kama hawana umeme wa kutosha.