Mlipuko wa volkeno
From Wikipedia
Mlipuko wa volkeno hutokea kama lava na gesi zinatoka vikali kwa nguvu.
Volkeno hupatikana pale ambako vipande vya ganda la dunia vinaachana au kusukumana. Kuna pengo ambako magma joto kutoka ndani ya dunia inapanda juu kufika usoni.
Mara nyingi volkeno hutoa lava yake mara kwa mara. Hii inawezekana kama njia ya kasoko yake ni wazi. Aina hii ya volkeno inaweza kuachana na nguvu yake mara kwa mara. Haielekei kuwa na mlipuko kali sana isipokuwa maji yanaingia katika chumba cha magma (soma chini).
Kama volkeno imelala kwa muda mrefu njia ya kasoko yake inafungwa kwa sababu lava ndani yake imeganda kuwa mwamba imara. Ikitokea ya kwamba joto la chini linaongezeka tena magma inaanza kupanda juu lakini haiwezi kutoka nje. Inakwama chini ya volkeno na shindikizo ndani yake inaongezeka. Kama shindikizo inazidi husababisha mlipuko na kutoka ghafla kwa lava na gesi nyingi mara moja. Ukali unaongezeka kama maji ya chini ya ardhi inaingia katika chumba cha magma chini ya volkeno.
Milipuko mikubwa ya aina hii iliwahi kurusha mlima wote hewani kwa mfano mlima wa Krakatau mwaka 1883 BK. Mlima mwenye urefu wa mita 813 juu ya UB ulipotea kabisa pamoja na kisiwa chake.
Ukitokea baharini mlipuko unaweza kusababisha mawimbi makubwa ya tsunami yanayofyeka mwambao.
Hatari nyingine ya milipuko ni kiasi kikubwa cha gesi na majivu. Gesi na majivu yenye halijoto hadi 800 °C zinaweza kusambaa haraka sana zikiteketeza kila kitu njiani. Pia gesi zinazotoka zinaweza kuwa za sumu. Wakati wa mlipuko wa Vesuvio watu wengi wa Pompei waliuawa na gesi pamoja na majivu.
Milipuko inaweza kutokea sambamba na tetemeko la ardhi.