Christopher Mtikila
From Wikipedia
Mchungaji Christopher Mtikila ni kiongozi wa chama cha upinzania Tanzania cha Democratic Party (DP).
Mtikila alizaliwa Iringa, kusini mwa Tanzania, mwaka 1950. Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa kanisa la kipentekoste la Full Salvation Church. Mchungaji Mtikila anajihusisha pia na harakati za haki za binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo kiitwacho Liberty Desk. Mwanzoni mwa miaka ya 90, mchungaji Mtikila alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu uhujumu wa uchumi unaofanywa na wahindi (ambao anawaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za Tanzania.
Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kutambua Zanzibar. Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na sio Tanzania. Hata hivyo Mtikila amebadili msimamo wake katika miaka ya karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama toka Zanzibar (kama sheria ya uchaguzi inayotaka) na hivyo chama chake kuweza kupata usajili wa kudumu. Mtikila alikuwa ni kati ya wagombea 10 wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Katika uchaguzi huo alipata kura asilimia 0.27.
Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali toka kwa Mkuu wa Wilaya na polisi.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba. Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala.