Panzi
From Wikipedia
Panzi ni aina ya mdudu anayekula mimea. Panzi wamo ndani ya Oda ya Orthoptera. Wanachupa mbali kwa kutumia miguu yao ya nyuma ambayo ina nguvu sana. Wengi wanaweza kuruka juu. Panzi wengine wana vipapasio vifupi na wengine wana vipapasio virefu. Panzi wakubwa na ambao wanajikusanya kwenye makundi wanaitwa nzige.
Panzi jike wenye vipapasio vifupi wana maumbile yanoyowawezesha kuchimba ardhi na kutaga mayai yao ndani ya vibumba. Vibumba vya mayai huweza kuwa na mayai zaidi ya kumi hadi zaidi ya mia moja. Mayai ya panzi aina nyingi huingia kwa diaposi kupitia majira ya baridi au kiangazi. Hali ya hewa ikiwa nzuri mayai yanaendelea kupevuka halafu tunutu wanatoka. Tunutu (panzi wachanga) huambua ngozi zao mara tano mpaka mara saba kufuatana na aina zao. Kila hatua ya ukuaji ni kubwa kuliko ile iliyotangulia. Hatua ya mwisho panzi mkubwa hutokea na kuwa mpevu ndani ya siku au wiki chache.
Kuna wadudu ambao wanafanana na panzi lakini wana vipapasio virefu kuliko miili yao. Aina moja kati yao anaitwa senene na huliwa na watu. Jike ana umbile kama mfuo kinachofanana na kitara. Anataga mayai juu ya au ndani ya mimea.
Panzi huliwa sehemu nyingi duniani kwa sababu wana virutubisho (protini) vingi. Wanajeshi huambiwa wakamate panzi na kuwala wakipungukiwa chakula.