Usimbishaji
From Wikipedia
Usimbishaji ni maji yanayonyesha kutoka hewa ardhini.
Maji haya ni pamoja na mvua, theluji, mvua mawe na umande.
Usimbishaji unaanza pale ambako hewa lenye joto na mvuke hupanda juu. Juu zaidi halijoto yake inapungua na mvuke ndani ya hewa unaanza kutonesha na kuwa matone ya maji. Kila wingu hufanywa na matone mengi madogo yanayoendelea kuelea hewani pamoja. Upepo inakoroga matone yale madogo mpaka yanagongana na kuunganika hivyo kukua.
Kama matone ni makubwa ya kutosha yanaanza kuanguka chini kama mvua, theluji au mvua mawe. Hali inategemea halijoto katika mawingu na hewani pale matone yanapotelemka.
Kiasi cha usimbishaji ni muhimu kwa ajili ya tabia za hali ya hewa katika nchi au eneo fulani.
[edit] Kufanya mvua kwa mitambo
Watu wameanza kufanya mvua kwa kukamua mawingu. Hapa punje ndogo za iodidi ya fedha zinatupwa mawinguni kwa njia ya ndege au makombora zinazokuwa viini vya kutonesha mvuke na kusababisha matone kukua hadi mvua kunyesha.
Teknolojia hii inatumika katika maeneo makavu. Yanatumika pia katika maeneo ya kilimo ili kuzuia mvua mawe isiharibu mavuno.