Ngugi wa Thiongo
From Wikipedia
Ngũgĩ wa Thiong'o (amezaliwa 5 Januari, 1938) ni mwandishi Mkenya aliyeandika kwa Kiingereza lakini siku hizi anatumia lugha ya Gikuyu. Maandishi yake ni pamoja na riwaya, tamthilia, hekaya, insha na uhakiki. Ameanzisha gazeti la lugha ya Gikuyu "Mutiiri". Tangu 1982 ameishi nje ya Kenya akifundisha kwenye vyuo vikuu mbalimbali kama Yale, New York na Irvine/California.
Contents |
[edit] Masomo
Ngugi amezaliwa Kenya katika kijiji cha Kamiriithu karibu na Limuru, wilaya ya Kiambu katika ukoo wa Wagikuyu akabatizwa James Ngugi. Alikuwa mtoto wa tano ya mke wa tatu wa babake Thiong'o wa Nducu. Baba alikuwa mkulima aliyepotea shamba lake kutokana na Waingereza kuteka na kutwaa Nyanda za Juu za Kenya. James alisoma shule za missioni za Kamaandura (Limuru), Karinga (Mangu) na Alliance High School (Kikuyu). Katika miaka ile akawa mkristo. Wakati aliposoma shule familia yake iliathiriwa na vita ya Maumau ikiwa kakaye aliuawa na mamake aliteswa.
Baada ya kumaliza Alliance High akasoma Makerere akachukua digirii ya Kiingereza mwaka 1963. Akafunga ndoa na Nyambura mwaka 1961 akazaa naye watoto sita katika miaka iliyofuata. 1962 aliandika tamthilia yake ya kwanza "The Black Hermit". Baada ya digrii alirudi Nairobi alipofanya kazi ya uandishi gazeti.
[edit] Riwaya za kwanza
1964 akachukua nafasi ya masomo huko Chuo Kikuu cha Leeds. Hapo Uingereza alitunga riwaya ya "WEEP NOT, CHILD" (1964) akiwa mwandishi wa kwanza kutoka Afrika ya Mashariki aliyetunga riwaya kwa Kiingereza. Alisimulia hadithi ya kijana Njoroge mwenye ndoto ya kuendeleza elimu yake lakini anakwama kati ya ndoto zake na hali halisi ya maisha ya Kiafrika chini ya ukoloni.
Aliendelea kwa "THE RIVER BETWEEN" (1965) akichora picha ya kijiji kilichopasuliwa kati ya wakristo na wafuasi wa dini ya asili. 1967 alitumia historia ya vita ya Maumau na maarifa ya familia yake kwa ajili ya riwaya ya "A GRAIN OF WHEAT".
Mwaka uleule baada ya kuchukua digrii ya pili alirudi Kenya akifundisha Chuo Kikuu cha Nairobi 1967-1969. Aliondoka kwa sababu alipinga kuingia kwa siasa ya serikali katika mambo ya chuo. Baada ya mwaka moja huko Makerere alipata nafasi ya kufundisha Marekani kwenye Chuo Kikuu cha Evanston (1970-71).
[edit] Profesa ya fasihi Nairobi
1973 alirudi Nairobi kama Profesa wa Kiingereza na mwenyekiti wa idara ya fasihi. Idara hii ilianzishwa kutokana na upinzani wa Ngugi na wenzake dhidi ya hali ya Kiingereza kuwa kitovuni mwa elimu katika Afrika. Katika makala 'On the Abolition of the English Department' aliyoandika 1968 pamoja na Taban lo Liyong and Henry Owuor-Anyumba aliwahi kuuliza "Tukihitaji kutazama historia ya utamaduni moja kwa undani kwa ajili ya masomo yetu kwa nini tusichague utamaduni mmoja wa Kiafrika na kuiweka kitovuni ili tulinganishe tamaduni mablimbali nao?" Kutokana na msimamo huo aliendelea kutafiti fasihi ya kimdomo ya makabila ya Kenya, hasa ya Wagikuyu na fasihi ya Kiswahili.
Katika miaka hii huko Nairobi Ngugi aliamua hawezi kuwa tena mkristo. 1976 akabadilisha jina lake kutoka James Ngugi kuwa Ngugi wa Thiong'o.
[edit] Fasihi ya kimdomo na gereza
Kazi yake ya kifasihi ilimpeleka katika mzozo na serikali. Kuanzia mwaka 1976 Ngugi alishirikiana na wanakijiji Wagikuyu karibu na Limuru kuanzisha maagizo ya tamthilia katika lugha yao. 1976 riwaya yake ya "PETALS OF BLOOD" ilichora picha ya watawala wapya Waafrika jinsi walivyochukua nafasi ya wakoloni wa awali wakidharau na kukandamiza wanachi. Mwaka uleule aliandika igizo la tamthilia "Ngaahika Ndeenda" (Nitaolewa nitakapopenda). Wakubwa katika serikali walikuwa na wasiwasi wakiogopa mwelekeo wa kimarxist wa Ngugu hasa alipotoka katika Chuo Kikuu na kuingia kati ya wananchi wa kawaida kwa njia ya maigizo yake katika lugha ya Gikuyu. Makamu wa Rais wa Kenya Moi aliamua kumkamata Ngugi chini ya sheria ya usalama wa kitaifa wakati Rais Jomo Kenyatta mwenyewe tayari alikuwa amedhoofika kutonana na uzee na magonjwa.
Ngugi alikaa mwaka moja katika gereza ya Kamiti akaandika riwaya ya kwanza kwa Gikuyu "Caitaani mũtharaba-Inĩ" (Shetani msalabani) akitumia karatasi ya choo. Baada ya kuachichwa hakuruhusiwa kurudi kazini kwenye chuo kikuu. Mwaka 1982 aliondoka Kenya kwenda London.
[edit] Maandishi ya baadye
Ngugi ameendelea kutumia Gikuyu pekee kwa ajili ya riwaya lakini amefundisha na kutunga insha kwa Kiingereza. Kati ya maandiko yaliyofuata ni "Detained" (Daiari ya gerezani - 1981); "Decolonizing the Mind: The Politics of Language in African Literature" (Kuondoa ukoloni rohoni - siasa ya lugha katika fasihi ya Afrika 1986) alimodai waandishi Waafrika watumie lugha zao za kienyeji badala la lugha za Kiulaya; Matigari (1987) alimotumia hadithi ya kiutamaduni wa Gikuyu.
Mwaka 2004 Ngugi alirudi mara ya kwanza Kenya lakini alipata maarifa mabaya akishambuliwa na wahuni na kuibiwa mali mke wake akibakiwa. Shabaha muhmu wa ziara yake ilikuwa kutangaza riwaya yake mpya kwa Gikuyu "Muroogi wa Kigogo".
Kiini cha imani ya Ngugi ni ya kwamba kwa kutumia lugha za kienyeji pekee waandishi waafrika watafikia wanachi wa kawaida na kushinda ukoloni mamboleo rohoni. Tatizo alilo nalo hapo ni ya kwamba lugha za kienyeji zinarudi nyuma haraka katika mazingira ya kisasa hata zikiendelea kuzungumzwa na kusikilizwa kwa redio si lazima zinasomwa pia.