Bantustan
From Wikipedia
Bantustan ilikuwa eneo katika Afrika Kusini wakati wa siasa ya Apartheid lililotenganishwa kama eneo la kabila fulani la Waafrika Weusi. Kimsingi ilikuwa kama rizavu katika koloni za Uingereza lakini chini ya siasa ya Apartheid ilitangazwa kuwa nchi ya pekee.
Contents |
[edit] Neno Bantustan
Neno Bantustan liliundwa na maneno "Bantu" (la kutaja Waafrika Weusi) na "-stan" (linalomaanisha kwa Kiajemi nchi ya watu fulani kama vile Uzbekistan = nchi ya Wauzbeki).
Maneno mengine yaliyotumiwa yalikuwa "homeland" (Kiingereza) na "tuisland" (Kiafrikaans).
[edit] Bantustan kama nchi huria kwa jina
Bantustan kumi zilitangazwa katika Afrika Kusini tena kumi nchini Namibia iliyotawaliwa na Afrika Kusini.
Bantustan kadhaa zilitangazwa kuwa nchi huria lakini hazikutambuliwa na umma wa kimataifa. Hizi zilikuwa:
- Transkei
- Venda
- Bophuthatswana
- Ciskei
Zingine zilipewa madaraka ya utawala wa ndani kama vile
- KwaZulu
- Lebowa
- QwaQwa
- Gazankulu
- KaNgwane
- KwaNdebele
Katika Namibia bantustan zifuatazo zilipewa madaraka ya utawala wa ndani:
- Ovamboland
- Kavangoland
- East Caprivi
[edit] Shabaha za siasa za Bantustan
Shabaha za kuundwa kwa maeneo haya zilielezwa waziwazi na chama cha NP. Waziri Connie Mulder alitangaza 1978: "Tutakapotimiza siasa yetu kuhusu watu weusi hatabaki mtu mmoja mweusi kama raia wa Afrika Kusini. Kila mtu mweusi atakuwa na uraia katika moja ya hizi nchi huria mpya kwa njia ya heshima. Bunge hii haitaskuwa tena na wajibu wa kuangalia watu hawa kisiasa."
Maana ya siasa hii ilikuwa kuhakikisha Afrika Kusini itaendelea kama nchi ya watu weupe hasa Maafrikaaner. Apartheid ilitaka kuondoa tatizo la watu weusi kuwa wengi nchini kwa kuwaondoa katika nchi kwa kuwahamisha katika Bantustan zilizotangazwa kuwa nchi za pekee tofauti na Afrika Kusini.
Kiini cha siasa hii ilikuwa pia ya kwamba bantustan zote zilipewa asilimia 13 tu ya eneo la Afrika Kusini na asilimia zaidi ya 80 zilitakiwa kubaki kama Afrika Kusini ya watu weupe. Hii ilimaanisha pia ya kwamba raia wa bantustan hizi hawakupata kazi na ajira kwao wakategemea kupata ajira katika Afrika Kusini - ila tu si kama wenyeji bali kama wageni walioweza kuondolewa na kushughulikiwa kama wageni yaani bila haki zozote hasa bila haki za kutafuta msaada wa mahakama. Kama mfano asilimia 65 za wafanyakazi wa Bophuthatswana walifanya kazi nje ya eneo lao.
[edit] Hali za Bantustan
Maisha katika Bantustan ilikuwa ya umaskini kwa watu wengi. Maeneo yalikuwa madogo mno na hasa maeneo yenye rutba yalibaki nje mkonono mwa wakulima makaburu. Siasa hii ya kuteua maeneo bila thamani tu kwa ajili ya Bantustan ilionekana pia kwenye ramani inayoonyesha Bophuthatswana na KwaZulu kama mkusaniyko wa vilaka si kama eneo la pamoja.
Hakuna Bantustan hata moja iliyoweza kujidumisha na zote zilitegemea misaada kutoka serikali ya Pretoria. Mwaka 1985 Transkei ilipokea 85% ya mapato yake kama ruzuku kutoka serikali ya Afrika Kusini.
Tatizo kubwa ya bantustan ilikuwa ufisadi wa viongozi na tabaka ya juu. Watu wachache walitajirika wakaweza kujenga maisha bora lakini idadi kubwa waliishi maskini mno. Wakubwa waliendesha biashara kama vilabu ambako raia wa Afrika Kusini waliweza kufurahia mambo yaliyokataliwa kwao: michezo ya kamari, biashara ya ngono na umalaya.
[edit] Mwisho wa Bantustan 1994
Mwisho wa Apartheid ilikuwa pia mwisho wa Bantustan zote zilizorudishwa ndani ya Afrika Kusini. Serikali kadhaa zilijaribu kupinga harakati hii lakini raia walisimama upande wa ANC.
Katika Bantustan ya Ciskei jeshi na polisi ya Afrika Kusini iliingilia kati mwaka 1994.