Utaridi
From Wikipedia
Utaridi ni sayari iliyo karibu na jua letu katika mfumo wa jua na sayari zake.
[edit] Jina la sayari
Jina lake limetokana na kiarabu عطارد (soma "`uTaarid") lakini asili yake ni katika lugha ya Babeli walioiita sayari ya kwanza kwa jina "Utarid" na kuiabudu kama mungu mmojawapo katika dini yao. Wagiriki walitumia jina la Apollo (ikionekana kama nyota ya asubuhi) au Hermes (ikionekana kama nyota ya jioni), Waroma jina la Mercurius na jina hili limeingia katika lugha nyingi za Ulaya. Umbo la kiarabu limekuwa jina la mtu katika nchi nyingi zilizoathiriwa na utamaduni wa Kiislamu pia jina la sayari ya kwanza kwa mfano kwa Kituruki au Kimalaysia.
Katika matumizi ya Kiswahili jina la Zebaki linaweza kupatikana lakini asili yake inaonekana ni kosa kutokana na jina la Kiingereza "Mercury". Mercury ni pia jina la metali inayoitwa zebaki kwa Kiswahili kutokana Kiarabu "زئبق" (tamka "zibaq").
[edit] Tabia za Utaridi
Utaridi ni sayari ndogo. Kipenyo chake kwa ikweta ni 4879.4 km. Kwa sababu iko karibu sana na jua ina mbio wa haraka. Mwaka wa Utaridi ambayo ni muda wa kuzunguka jua ni siku 88 za dunia pekee.
Inazunguka kwenye kipengo chake katika muda wa siku 58.6 za dunia. Kutokana na kuwa karibu na jua kuna joto kali upande unaotazama jua lakini upande wa usiku ni baridi kabisa kutokana na uhaba wa hewa inayoweza kutunza halijoto. Halijoto ya wastani ni +178.8 °C, (usiku -183.15 °C na mchana +426.85 °C).
Uhaba wa hewa umesababisha uso wa sayari kujaa mashimo ya kasoko. Kasoko hizi zimesababishwa kwa kugongwa na meteoridi. Ganda la hewa kama duniani lingeangamiza meteoridi ndogo na kusababisha kupasuka kwa kubwa lakini zote zinafika usoni wa Utaridi bila kizuizi. Alama za meteoridi ni mmomonyoko wa pekee unaoonekana hakuna dalili ya mmomonyoko kutokana na hewa au maji ya awali.
Kutokanana na kuwa karibu sana na jua Utaridi inaonekana kama nyota kwa macho katika masaa ya pambazuko na machweo pekee.
Mfumo wa jua na sayari zake |
---|
Jua - Utaridi - Zuhura - Dunia (Mwezi) - Meriki - Mshtarii - Zohari - Uranus - Neptun |