Gandunia
From Wikipedia
Gandunia (kutoka maneno "ganda" na "dunia") ni mafundisho ya sayansi za jiolojia na jiofizikia kuhusu tabia za ganda la dunia na miendo ya sehemu zake.
[edit] Muundo wa dunia
Inaanza na hoja la kuwa muundo wa dunia ni wa tabaka mbalimbali. Tabaka imara ni ganda la nje la dunia pamoja na sehemu ya juu ya koti ya dunia chini ya ganda hili. Tabaka hii -inayoitwa "tabakamwamba"- inakaa juu ya tabaka moto na laini.
Ndani ya tabaka hili laini kuna mwamba katika hali ya geli yaani ni kati ya hali imara na hali kiowevu. Kwa hiyo vipande vyake havikai mahali pamoja lakini vina mikondo ndani yake kufuatana na mikondo ya joto kali inayopanda juu kutoka kiini cha dunia ambacho ni chuma ya moto katika hali kiowevu.
Mikondo hii inasukuma dhidi ya tabakamwamba ya nje na kuivunjavunja katika mabamba mbalimbali.
[edit] Mwendo wa mabamba
Kufuatana na nadharia ya gandunia sehemu za ganda la nje la dunia yetu zina mwendo wakati wote. Mwendo huu husababishwa na kupaa juu kwa magma (yaani mwamba moto wa kiowevu) inayotoka nje kwenye migongo iliyoko katikati ya msingi wa bahari. Migongo hii ni safu ya milima ya kivolkeno chini ya maji, kwa mfano mgongo kati wa Atlantiki.
Magma hii inapoa kuwa mwamba mpya na kusukuma nusu mbili za bamba la kibahari kwenda nje. Pale ambako bamba la kibahari inapokutana na bamba la bara linajisukuma chini yake kwa sababu miamba ya mabara ni nyepesi na miamba ya bamba la kibahari ni nzito zaidi. Hivyo pembizo la bamba la kibahari linazama chini na kuyeyuka katika joto la koti ya dunia. Eneo la kuzama chini linanonekana mara nyingi kama mfereji chini ya bahari.
Shindikizo hili la msingi wa bahari linasababisha pia mwendo wa bamba la kibara pamoja na kuvunjika kwa mabamba ya kibara.
[edit] Gandunia na uso wa dunia
Miendo ya gandunia imeunda uso wa dunia jinsi ilivyo na jinsi inavyoendelea kutokea na kubadilika.
- kugongana kwa mabamba husababisha kukunja kwa ganda la dunia na kutokea kwa nyororo za milima.
- Mfano: Safu ya milima ya Himalaya - imejikunja kutokana na bamba la Uhindi kujisukuma dhidi ya bamba la Asia
- kuzama kwa pembizo la bamba moja chini ya bamba lingine husababisha kutokea kwa mifereji chini ya bahari na volkeno kwenye bamba la juu - au kutokea kwa nyororo ya visiwa vya kivolkeno kwenye mstari wa kuzama. Maeneo haya kuna mitetemeko ya ardhi mara kwa mara.
- Mfano: Visiwa vya Antili Ndogo (sehemu ya kusini ya pinde la Visiwa vya Karibi) vinafuatana na pembizo la bamba la Karibi linapogongana na bamba la Amerika Kusini. Visiwa vyote ni vya asili ya kivolkeno yaani kila kisiwa ni sehemu inayoonekana ya mlima wa volkeno unaoanza chini ya bahari.
- shindikizo ya gandunia husababisha pia kuvunjika kwa mabamba. Hali hii inaonekana kwa kutokea kwa mabonde ya ufa.
Makala hiyo kuhusu "Gandunia" bado ni mbegu. Unaweza kusaidia kuikuza kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Ikiwepo makala kuhusu Gandunia kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |
Categories: Jiolojia | Gandunia | Sayansi za dunia | Jaribio | Mbegu