Bamba la gandunia
From Wikipedia
Bamba gandunia ni kipande kikubwa cha ganda la dunia lenye mwendo wake wa pekee pamoja na au dhidi ya mabamba gandunia mengine.
Mabamba haya ni sehemu ya nje ya tabakamwamba (lithosferi). Tabaka hili limevunjika katika vipande vikubwa 7 na vingine vidogo vinavyoelea juu ya tabaka lenye hali ya kiowevu chenye mnato mzito.
Mabamba haya yote yameonekana kuwa na mwendo wa sentimita kadhaa (2 - 20 cm zimepimwa) kwa mwaka. Mwendo huu husababishwa na nguvu ya magma (mwamba moto wa kiowevu) inayopanda juu na kusukuma mabamba haya. Ulinganisho ni kama vipande vya ganda inayotokea juu ya maziwa vinaanza kuonyesha mwendo kama sufuria ya maziwa imepashwa moto.
[edit] Mabamba makuu ya dunia
Mabamba makubwa ya ganda la nje ya dunia ni:
- Bamba la Afrika - bara la Afrika pamoja na tako la bara baharini - ni bamba la kibara
- Bamba la Antaktika - bara la Antaktika pamoja na tako la bara baharini - ni bamba la kibara
- Bamba la Australia - bara la Australia pamoja na tako la bara baharini - ni bamba la kibara
- Bamba la Ulaya-Asia - mabara ya Ulaya na Asia pamoja na tako la bara baharini - ni bamba la kibara
- Bamba la Amerika ya Kaskazini - bara la Amerika ya Kaskazini na Siberia ya kaskazini-magharibi pamoja na tako la bara baharini - ni bamba la kibara
- Bamba la Amerika ya Kusini - bara la Amerika ya Kusini pamoja na tako la bara baharini - ni bamba la kibara
- Bamba la Pasifiki - bahari ya Pasifiki - ni bamba la kibahari
Kati ya mabamba madogo ni:
- Bamba la Uhindi
- Bamba la Uarabuni
- Bamba la Karibi
- Bamba la Juan de Fuca
- Bamba la Skotia
[edit] Mendo wa mabamba
Mwendo wa mabamba haya umesababisha kutokea na kuvunjika kwa mabara katika historia ya dunia yetu.
Wataalamu hufikiri ya kwamba dunia ilikuwa na bara kubwa moja tu (Pangaea) miaka milioni 300 - 150 iliyopita iliyovunjika katika vipande au mabamba mbalimbali.
Hata mabamba yaliyopo kwa sasa yanategemewa kuendelea kuhamahama, kuvunjika au kupotea kabisa.
Kwa mfano Afrika iko katika mwenendo wa kupasuliwa kwenye mstari wa Bonde la Ufa yaani Afrika ya Mashariki inaelekea kujitenga na sehemu nyingine ya bara ikiwa bamba la pekee. Penye Bonde la Ufa la sasa bahari itatandiwa baada ya miaka milioni 20.
Bara Hindi au bamba la Uhindi inaendelea kusukuma dhidi ya bamba la Asia na kujisukuma chini ya milima ya Himalaya - kuna uwezekano ya kwamba itaingia kabisa na kutoweka.
Categories: Jiografia | Jiolojia | Gandunia | Jaribio