George Weah
From Wikipedia
George Weah ni mwanakandanda mashuhuri duniani na mwanasiasa aliyegombea urais wa Liberia mwaka 2005. Weah alizaliwa Oktoba 1, 1966 katika jiji la Monrovia. Alikulia katika kitongoji cha masikini cha Clara. Kabla ya kujiunga na soka la kulipwa Weah alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Mawasiliano la Liberia kama fundi simu.
Kielimu, Weah ana Shahada ya Kwanza ya Uendeshaji Michezo toka Chuo Kikuu cha Parkwood, Londo, Uingereza. Mwkaa 1999 alipata shahada ya Udakitari ya Heshima toka Chuo Kikuu cha A.M.E Zion nchini Liberia.
Mwaka 1995 Weah alipewa tuzo na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa Mwanasoka Bora Duniani. Yeye ni mwanasoka pekee toka Afrika aliyewahi kupewa tuzo hiyo. Mwaka huo huo alichaguliwa pia kuwa Mwanasoka Bora Ulaya na Mwanasoka Bora Afrika.
Weah alianza safari yake ya soka katika timu ya Liberia ya Incincible Eleven na Tonnerre Yaounde, ya Cameroon. Baada ya hapo alikwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya mwaka 1988. Alijiunga na timu ya Monaco ambapo aliiongoza kushinda kombe la Ufaransa mwaka 1991. Baadaye alijiunga na [[Paris Saint Germain mwaka 1992-95. Aliiongoza timu hii kuchukua kombe la ligi ya Ufaransa mwaka 1994. Mwaka 1995-2000 alikuwa akiichezea timu ya AC Milan ambayo ilishinda ligi ya Italia mwaka 1996 na 1999. Mwaka 2000 aliondoka AC Milan na kujiunga na Chelsea, baada ya muda mfupi alijiungana Manchester City na baadaye Marseille mwaka 2001. Alimaliza soka la kulipwa akiwa na timu ya Al JAzira ya Falme ya Nchi za Kiarabu.
Weah amekuwa akitoa misaada kusaidia wananchi wa Liberia. Mwaka 2004 alipewa tuzo ya Arthur Ashe kwa juhudi zake za kusaidia kujenga nchi yake.