Kumbukumbu la Sheria
From Wikipedia
Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria ni kitabu cha tano katika Agano la Kale au Biblia ya Kiebrania. (Kitabu cha kwanza ni Mwanzo.) Kwa asili kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa Devarim, maana yake “maneno”, ambalo ni nomino ya kwanza katika kitabu hicho. Wengine wanakiita Kitabu cha Tano cha Mose (au Musa) kwa vile inafikiriwa kuwa Mose ni mwandishi wa kitabu hicho. Kwa lugha ya Kilatini, kinaitwa Deuteronomium, maana yake “Sheria ya Pili (au Nyingine)”.
Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria kina sura thelathini na nne, na karibu sura zote zinasimulia hotuba tatu za Mose kwa Waisraeli. Ni sura nne za mwisho tu zinazohusu mambo ya kihistoria: Yoshua ameteuliwa kumfuata Mose kama kiongozi wa taifa (sura 31), Mose anaimba wimbo wake wa mwisho (sura 32), baraka ya Mose kwa makabila 12 ya Israeli (sura 33), na mwishoni habari za kifo chake Mose (sura 34.)