Volkeno
From Wikipedia
Volkeno (pia: volkano, zaha) ni mahali ambako lava inatoka nje kwa uso wa ardhi. Mara nyingi -lakini si kila mahali- volkeno ni mlima. Volkeno huwa na kasoko yaani shimo ambako lava na gesi inatoka nje.
Volkeno ni dalili ya kwamba mahali pake ganda la dunia si nene sana hivyo joto la ndani linapata njia ya kutoka nje. Volkeno huanza katika tambarare. Lava hutoka katika hali ya kiowevu ikipoa haraka inaganda kuwa mwamba na hujenga mlima wa kuzunguka shimo la kasoko yake. Milima ya aina hii inaweza kukua sana. Mfano wa volkeno kubwa ni Kilimanjaro. Miamba yake yote ilijengwa na lava iliyotoka ndani ya dunia.
Volkeno nyingi hutokea pale ambako mabamba ya ganda la dunia vinaachana au kusukumana. Hivyo volkeno hutokea hasa kwenye mistari ya kukutana kwa mabamba haya.
Sababu nyingine ya kutokea kwa volkeno ni kuwepo kwa chumba cha magma ndani ya ganda la dunia.
Mlipuko wa volkeno ni hatari sana kwa ajili ya wanadamu na mazingira. Kuna mifano ya vifo vingi vilivyosababishwa na volkeno. Hasara inategema kama miji iko karibu na volkeno au la, na kama serikali zina huduma za kutazama volkeno na kuonya watu watoke mapema wakati dalili za kwanza zinatokea.
Kati ya mifano ya milipuko makali inayojulikana zaidi ni:
- mlipuko wa volkeno ya Vesuvio, Italia. Iliharibu miji ya Pompei na Herkulaneo mwaka 79 BK.
- mlipuko wa volkeno ya Krakatau, Indonesia mwaka 1883. Ilirusha vumbi nyingi angani kiasi kilichoonekana kote duniani
- mlipuko wa volkeno Nevado del Ruiz, Kolumbia mwaka 1985 uliua watu 25.000 kutokana na kuyeyusha theluji na barafu mlimani na kusababisha mafuriko ya ghafla
Ol Doinyo Lengai ni volkeno ndogo iliyolipuka Tanzania kaskazini mwaka 2006.
![]() |
Makala hiyo kuhusu "Volkeno" bado ni mbegu. Unaweza kusaidia kuikuza kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Ikiwepo makala kuhusu Volkeno kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |