Hawaii
From Wikipedia
Hawaii ni funguvisiwa ya Pasifiki ambayo ni jimbo la Marekani, pia ni jina la kisiwa chake kikubwa.
Hawaii ilikuwa ufalme wa Wapolynesia ikawa koloni ya Marekani katika karne ya 19 na imekuwa jimbo la Marekani tangu 21 Agosti 1959. Mji mkuu ni Honolulu kwenye kisiwa cha Oahu.
[edit] Jiografia
Funguvisiwa ya Hawaii ina jumla ya visiwa 137 vyenye eneo la kilomita za mraba 16,649 za nchi kavu. Visiwa vilivyo vingi ni vidogo, havikaliwi na watu.
Visiwa vikubwa ni kuanzia upande wa magharibi kwenda mashariki:
- Niʻihau
- Kauaʻi
- Oʻahu
- Molokaʻi
- Lānaʻi
- Kahoʻolawe
- Maui
- Hawaiʻi
Visiwa vyote vina asili ya kivolkeno. Mlima Mauna Kea ni volkeno ndefu kabisa duniani yenye kimo cha 4201 m juu ya UB lakini inaanza chini ya bahari katika kina cha 5,000 m hivyo kimo cha jumla ni zaidi ya 9,000 m. Volkeno ya pili ni Mauna Loa yenye masi kubwa zaidi. Mauna Loa ni volkeno hai kwenye kisiwa kikuu cha Hawaii, pamoja na mlima Kilauea.
[edit] Historia
Hawaii ilikaliwa na Wapolynesia waliofika kwa mitumbwi yao mikubwa. Jamii zao zilitawaliwa na familia za makabaila zilizotazamiwa kuwa hali ya juu kuliko watu wa kawaida. Tabaka la pili la juu walikuwa makuhani.
Kati ya 1781 na 1811 Kamehameha I alifaulu kuunganisha visiwa vyote chini ya utawala wake akawa mfalme wa kwanza wa Hawaii yote.
Katika miaka ya karne ya 19 iliyofuata wageni kutoka Marekani na Ulaya walianza kujenga makazi visiwani. Uchumi wa kisasa ulianzishwa kwa mashamba ya miwa na uvuvi. Mwaka wa 1842 Marekani ikatambua ufalme wa Hawaii kama nchi huru ya kujitegemea.
Athira ya wafanyabiashara matajiri Wazungu ikakua. Kwa njia ya ghasia wakamlazimisha mfalme Kalakaua mwaka 1887 kukubali katiba iliyowapa haki ya kupiga kura matajiri pekee. Mwaka uleule Marekani ilipewa haki ya kutawala kituo cha kijeshi cha Pearl Harbour.
Malkia Liliuokalani († 1917) alijaribu mwaka 1893 kufuta katiba na kurudisha mamlaka ya wafalme lakini alipinduliwa na wenye mashamba makubwa waliosaidiwa na wanajeshi wa Marekani, na jamhuri ya Hawaii ikatangazwa.
Wakati wa Vita ya Marekani dhidi Hispania serikali ya Marekani iliamua kutwaa Hawaii na kuitangaza kuwa mali ya Marekani. Baadaye visiwa vilitawaliwa kama koloni na baadaye kama eneo la kitaifa la Marekani.
Marekani iliingia katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa shambulio la Japani dhidi ya manowari za Marekani katika bandari ya Pearl Harbour tar. 7 Desemba, 1941.
Mwaka 1959 Hawaii imekuwa jimbo kamili la Marekani.
Template:Marekani
Makala hiyo kuhusu "Hawaii" bado ni mbegu. Unaweza kusaidia kuikuza kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Ikiwepo makala kuhusu Hawaii kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |