Karthago
From Wikipedia
Karthago (Kilatini Carthago, Kigiriki Καρχηδών Karchēdōn; katika lugha asilia ya Kifinisia Qart-Hadašt, yaani "mji mpya") ilikuwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita mji mkubwa katika Afrika ya Kaskazini karibu na Tunis ya leo nchini Tunesia.
Karthago iliundwa na Wafinisia kutoka pwani la Shamu na Lebanon kama koloni. Ikakua kuwa mji mkubwa kabisa katika magharibi ya Mediteranea. Ilitawala maeneo ya pwani katika nchi za leo za Libya, Tunesia, Algeria, Moroko, Hispania, Ureno na Ufaransa pamoja na visiwa vikubwa vya Mediteraneo.
Baada ya kuvamiwa na Dola la Roma mwaka 146 KK Karthago ikawa mji wa Kiroma. Kati ya 439 hadi 533 ilikuwa mji mkuu wa ufalme wa Wavandali katika Afrika ya Kaskazini halafu ikarudi chini ya Bizanti.
Waarabu Waislamu walipovamia Afrika ya Kaskazini mwaka 647 Karthago ilikuwa na kuta na boma imara sana ikafaulu kujitetea hadi mwaka 698 BK. Baada ya kuteka mji Waarabu waliamua kutumia majengo yake kama windo la mawe. Nyumba nyingi za mji wa Tunis zimejengwa na mawe ya Karthago ya zamani.