Uislamu
From Wikipedia
Uislamu ni dini inayotokana na mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W.). Waislamu wanaamini kuwa mafunzo yaliyoko kwenye Kurani; kitabu mwongozo cha dini hii, yanatokana na ujumbe aliopewa Muhammad na Mungu (Allah S.W.) kupitia malaika Jibrili.
Uislamu unazungumzia kuhusu upweke na umoja wa Mwenyezi Mungu aliyetukuka, na itikadi ya kila Muislamu ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Muumba asiyekuwa na mshirika, hana baba wala mwana, hakuzaa wala hakuzaliwa, na hana mwanzo wala mwisho.
Contents |
[edit] Mafunzo ya Uislamu
Uislamu unawafunza wafuasi wake mambo mengi yanayohusiana na maisha, ikiwa yale yanayohusu ibada kama Sala, Zaka, Saumu na Hija; ambazo pamoja na kauli ya Shahada (Nakiri kwa moyo na kubain kwa ulimi kwamba hakuna Mola apsaye Kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni Mtume wake) huitwa nguzo za Uislamu au yale yanayohusu maingiliano baina ya wanadamu, yakiwa maingiliano ya kijamii kama ndoa na talaka na ujirani mwema, au ya kiuchumi kama biashara, au ya kisiasa kama kawaida za kumchagua kiongozi wa dola, au ya uhusiano baina ya mataifa mbali mbali ulimwenguni. Uislamu ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu, kiimani, kimaisha, kisiasa, kijamii na kiuchumi.
[edit] Ibada katika Uislamu
Ibada katika Uislamu ni vile vitendo vinavyofanywa na Muislamu kumfanyia Mwenyezi Mungu tu peke yake, kwani ibada yoyote haitakikani iwe na ushirikina ndani yake, na wakati itakapokuweko aina yoyote ya shirki basi ibada ile inakuwa haina maana wala hapana thawabu wala ujira wowote unaopatikana, na inakuwa ni kazi ya bure. Kwa hivyo, kila Muislamu anatakikana wakati anapofanya ibada yake afanye kwa ajili ya Mola wake aliyemuumba akampa kila aina ya neema na kumtukuza kuliko viumbe vyengine vyovyote, kwa kumpa akili na fahamu na elimu.
[edit] Aina za ibada katika Uislamu
Nguzo tano za Uislamu: Nguzo za Uislamu ni tano.
- Shahada: Nguzo ya kwanza ya Uislamu ambayo hujumuisha kutoa kauli mbili: Hakuna Mola apsaye Kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni Mtume wake. Kauli hii hutolewa pale mwanadaamu anapoingia Uislamu. Kila Muislamu anapaswa kutoa shahada.
- Sala: Nguzo ya pili ya Uislamu na ni ibada muhimu kabisa ambayo inampa fursa Muislamu kuingia katika ukumbi wa Mwenyezi Mungu na kuzungumza naye na kumuomba na kumtaka haja zake.
- Zaka: Nguzo ya tatu ya Uislamu nayo ni ibada inayomuelekeza Muislamu kuwaangalia Waislamu wenzake kwa hali na mali, na kushughulikia mahitajio yao ya maisha, kwa kutoa fungu la mali yake na kuwapa wale walio maskini na wasiojiweza ili na wao waweze kuishi uzuri
- Funga/Swaum: Nguzo ya nne ya Uislamu nayo ni ibada inayomkurubisha Muislamu na Mola wake na kumfanya amche na kumuogopa zaidi, kwani saumu humsaidia Muislamu kufahamu shida na taabu ambazo wale wasiokuwa na uwezo wanazipata wakiwa na njaa na hawana cha kukila, na kwa hivyo, huingiwa na huruma na kuwa na moyo wa kutaka kuwasaidia na kuwaondoshea shida hii.
- Hija: Nguzo ya tano na ya mwisho ya Uislamu, ambayo inawapa fursa Waislamu ulimwenguni kukutana na wenziwao na kujua hali zao na kupata nafasi ya kuomba maghfira na msamaha kwa madhambi yao katika mkutano mkubwa kabisa wa wanadamu ulimwenguni.
[edit] Maingiliano katika Uislamu
Uislamu umeweka kawaida mbali mbali katika maisha wakati watu wanataka kuweka uhusiano fulani baina yao ili mambo yende kwa uzuri na uhusiano uzidi kuwa mwema baina yao. Katika maingiliano yaliyowekewa kawaida na nidhamu katika Uislamu ni mambo yanayohusu:
1- Nikaha au ndoa baina ya Waislamu 2- Biashara na mambo yanayohusu uchumi 3- Uhusiano wa kijamii baina ya watu katika mtaa au kijiji au mji au nchi 4- Uhusiano wa kimataifa baina ya madola mbali mbali, yakiwa ya kiislamu au yasiyokuwa ya kiislamu.
[edit] External Links
- cennet - Uislamu Kurasa za pekee
- Islam Blog