Kalenda ya Kiislamu
From Wikipedia
Kalenda ya Kiislamu ni mtindo wa kuratibu wakati unaopatikana katika nchi mbalimbali za Kiislamu. Pia Waislamu wanaoishi katika mazingira isiyo ya kiislamu hutumia kalenda hii kwa ajili ya kupanga maisha yao ya kidini, hasa sikukuu na saumu. Mahali pengi Kalenda ya Kiislamu hutumika pamoja na kalenda zinazofuata mwendo wa jua, hasa kalenda ya kikristo.
Contents |
[edit] Miezi na mwaka
Kalenda ya Kiislamu imepokea kawaida ya mwaka wa Waarabu wa kale: mwaka una miezi 12.
"Mwezi" humaanisha kipindi kamili kati ya kuonekana kwa mwezi angani mara ya kwanza (hilal) hadi kurudia kwa kuonekana kwake. Kwa sababu muda wa kipindi hiki ni siku 29,5 mwezi halali huhesabiwa kuwa na siku 29 au 30. Kipindi kinachoitwa "mwezi" katika kalenda ya kikristo hakina uhusiano tena na mwezi halisi.
Waislamu wanaofuata mfano wa Kisaudi hukubali mwezi mpya umeanza kama umeonekana kwa macho. Kwa sababu desturi hii imeleta matatizo ya kutokubaliana pia ni rahisi kukadiria mwendo wa mwezi nchi mbalimbali za kiislamu hutumia makadirio ya kitaalamu kupanga tarehe za miezi.
Idadi ya siku katika mwaka wa kiislamu ni 354.
[edit] Hesabu ya miaka
Taz. makala "Miaka baada ya hijra"
Hesabu ya miaka katika kalenda ya Kiislamu hufuta utaratibu wa "miaka baada ya hijra" tangu kuhamia kwake Mtume Muhammad kutoka Makka kwenda Madina. Hijra ilitokea mwaka 622 BK au katika mwaka 1 wa hesabu yenyewe.
Njia inayofuata inasaidia kujua takriban tarehe gani ya kiislamu inalingana na tarehe ipi katika kalenda ya kikristo:
- K = (32H : 33) + 622
- H = {33*(K - 622)): 32
K (Mwaka "baada ya Kristo" katika kalenda ya Kikristo), H (Mwaka "Baada ya Hijra" katika kalenda ya Kiislamu)
Kati ya nchi za Kiislamu Uajemi na Afghanistan hutumia mwaka wa jua wakihesabu tangu hijra. Lakini pamoja na kalenda hii wanatumia mwaka wa kimwezi wa kiislamu kwa kupanga sikukuu za kidini.
[edit] Miezi
Miezi yenye sikukuu muhimu ni hasa mwezi wa saumu wa Ramadhani, mwezi wa Haj mwenye tar. 10 ndiyo Idd-ul-fitri na mwezi wa Rabi' ul-auwali mwenye tar. 12 Idd-ul-maulidi yaani sikukuu ya kuzaliwa kwake Mtume Muhammad (Maulidi-an-Nabii).
Mwezi wa Muharram ni muhimu sana kati ya Washia wanaokumbuka mateso na kifo cha Imam Husain wakati wa mapigano ya Karbala.
Majina na ufuataji wa miezi ni hivi:
- Muharram محرّم
- Safar صفر
- Rabi`-ul-Awwal (Rabi' I) ربيع الأول
- Rabi`-ul-Akhir (Rabi' II) ربيع الآخر أو ربيع الثاني
- Jumaada-ul-Awwal (Jumaada I) جمادى الأول
- Jumaada-ul-Akhir (Jumaada II) (Jumaada II) جمادى الآخر أو جمادى الثاني
- Rajab رجب
- Shaaaban شعبان
- Ramadan رمضان
- Shawwal شوّال
- Dhul Qaadah ذو القعدة
- Dhul Hijjah ذو الحجة
[edit] Siku za Juma au Wiki
Kalenda ya Kiislamu hutumia juma au wiki ya siku saba jinsi ilivyo kawaida hata kwa Wayahudi au Wakristo. Siku muhimu zaidi ni Ijumaa ambako Waislamu hukunsanyika kwa ajili ya sala ya pamoja.
Kwa kiarabu majina ya siku za juma hufuata hesabu ya Kiyahudi jinsi inavyoonekana katika Biblia. Jumapili inaitwa "siku ya kwanza", Jumatatu "siku ya pili" hadi "siku ya tano" = Alhamisi. Siku ya sita pekee imepewa jina jipya la Kiislamu kutokana na mkutano wa sala ya pamoja. Siku ya saba tena imebaki na jina lake la kibiblia Sabato au siku ya saba. Hii ni kwa sababu utamaduni wa kiarabu kabla ya Uislamu uliwahi kupokea athira nyingi kutoka kwa Wayahudi na Wakristo pia walikuwepo Waarabu wakristo na wayahudi.
Majina ya siku katika lugha ya Kiswahili yanaonyesha ya kwamba lugha ilianza katika mazingira ya kiislamu kabisa bila athira za moja kwa moja kutoka Uyahudi au Ukristo. Majina ya siku yamepangwa kufuatana na Ijumaa ambayo ni siku muhimu hasa katika maisha ya kiislamu. Maana ya Jumamosi, Jumapili n.k. ni "Siku ya kwanza, pili, tatu" baada ya Ijumaa. Alhamisi imebaki na jina la kiarabu.
- Jumapili: yaum al-ahad (siku ya kwanza) يوم الأحد
- Jumatatu: yaum al-ithnayna (siku ya pili) يوم الإثنين
- Jumanne: yaum ath-thalatha (siku ya tatu) يوم الثلاثاء
- Jumatano: yaum al-arba`a (siku ya nne) يوم الأَربعاء
- Alhamisi: yaum al-khamis (siku ya tano) يوم خميس
- Ijumaa: yaum al-jum`a (siku ya mkutano) يوم الجمعة
- Jumamosi: yaum as-sabt (siku ya sabato) يوم السبت